Leo katika kipengele hiki tutaona jinsi ya kukabiliana na changamoto hii. Lakini kabla hatujaona ni nini cha kufanya, hebu tusome maoni ya msomaji mwenzetu.
Nilikuwa nimeajiriwa na Wazungu fulani. Walipoondoka nilianza kigenge cha laki mbili sasa naendelea mdogo mdogo. Changamoto yangu ni kukuza na kupata duka la jumla. tatizo ni wapi nitapata mtaji usiozidi milioni kufikisha malengo yangu, nitumie njia gani maana kigenge changu pato lake halizidi 40 kwa siku, naomba ushauri nifanyeje. M.P
Kama tulivyosoma alichoandika msomaji mwenzetu hapo juu, ameanza biashara na mtaji kidogo na sasa changamoto yake ni kuikuza biashara hiyo zaidi. Hapa tutashirikishana baadhi ya mambo ya kufanya ili kuweza kukuza biashara hii na kufikia mafanikio makubwa.
1. Jipe muda, biashara haitaweza kukua haraka kama unavyofikiri
Uzuri wa kuanza biashara na mtaji kidogo ni kwamba kila mtu anaweza kufanya hivyo. Lakini pia urahisi huu wa kuanza biashara kwa mtaji kidogo unafanya ukuaji wa biashara kuwa wa taratibu sana. Hivyo unapofanya biashara yoyote ambayo unaanza na mtaji kidogo ni muhimu ukajipa muda ili kuweza kukuza mtaji wako. Usiwe na tamaa ya kutaka kukuza biashara hii haraka, unaweza kuingia kwenye maamuzi ambayo yatakugharimu zaidi. Endelea kufanya biashara yako huku ukijifunza zaidi na kuangalia kila fursa ambayo unaweza kuitumia kukuza biashara yako.
2. Kuza mtaji wako taratibu
Kwa mtaji huo mdogo ambao umeanza nao biashara, endelea kuukuza kila siku. Usiendeshe biashara kwa kula kila kipato unachopata, badala yake tenga sehemu ya akiba irudi kwenye biashara yako. Fanya hivi kwa nidhamu ya hali ya juu sana na unahakikisha kila unapopata faida sehemu inarudi kwenye biashara yako. Pia endelea kuangalia kwa mazingira uliyonayo na kwa biashara unayofanya ni kwa jinsi gani unaweza kukuza mtaji wako zaidi. Kama utafikiria hili kila siku, hutakosa majibu ambayo yatakusaidia.
3. Punguza gharama za biashara na za maisha pia
Kuwa kwenye biashara haimaanishi kwamba ndio una uhuru wa kufanya chochote unachotaka na fedha za biashara hiyo, kwa sababu tu ni zako. Wewe sasa upo kwenye wakati mgumu wa kukuza biashara yako huku ukiwa huna njia nyingi za kufanya hivyo. Hebu kwa sasa punguza kabisa gharama zako za kibiashara na za maisha pia. Kama kitu sio muhimu sana basi usikigharamie. Punguza matumizi yote ambayo ni ya anasa tu na sio kwa ukuaji wa biashara. Katika kupunguza gharama zako za biashara na maisha, jijengee nidhamu nzuri sana ya fedha. Usitumie fedha kiholela tu, kuwa na mahesabu na sababu kwa nini umetumia fedha fulani, hasa kwa matumizi ambayo sio ya kawaida.
4. Angalia watu ambao unaweza kushirikiana nao
Baada ya kuiendesha biashara yako vizuri na ukaona inaenda kwa faida, unaweza kuangalia watu ambao unaweza kushirikiana nao kwenye biashara hiyo. Kuna watu wengi ambao wanaweza kuwa na mtaji lakini hawana muda wa kufanya biashara. Lakini pia watu hawa wanataka mtu ambaye wanaweza kumwamini. Hivyo kama unaweza kuaminika angalia watu unaoweza kushirikiana nao kibiashara. Andaa mpango mzuri ambao utamshawishi mtu ni jinsi gani yeye atafaidika kama atawekeza kiasi kidogo kwenye biashara yako. Ikiwa unaendesha biashara yako kitaalamu itakuwa rahisi zaidi kushawishi watu kushirikiana na wewe.
5. Rasimisha biashara yako ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata mkopo
Hata kama biashara yako ni ndogo kiasi gani, irasimishe. Iendeshe kisheria kwa kuwa na namba ya mlipa kodi na hata leseni pia. Hivi vitakuwezesha wewe kutambulika na taasisi za kifedha pale utakapohitaji msaada zaidi wa kifedha. Mkopo kwenye taasisi za kifedha ni chanzo muhimu ila usikimbilie kama bado hujaweza kuiendesha biashara yako kwa faida. Hakikisha umeiweka biashara yako vizuri kwanza na inajiendesha kwa faida ili unapochukua mkopo unajua unauweka wapi na kuendelea kupata faida zaidi. Kuikuza biashara pale ambapo umeanza na mtaji kidogo ni kitu ambacho kinawezekana. Ila unahitaji kujitoa na kujenga nidhamu kubwa. Unahitaji kufanya kazi zaidi ya wafanyabiashara wengine, unahitaji kuwa mbunifu wa hali ya juu na pia unahitaji kujijengea uaminifu. Ukishajua wewe biashara yako ni ndogo na inahitaji kukua, basi hakikisha kila mara unaumiza akili yako ifikirie njia zaidi za kuikuza. Na kama utaweza kufanya hivi basi utaziona fursa nyingi zilizokuzunguka za kuikuza biashara yako.
No comments:
Post a Comment